ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, October 14, 2017

TAMASHA LA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA ARUSHA KUFANYIKA KESHO


 
wakwanza kulia ni Katibu wa TASWA mkoa wa Arusha, Mussa Juma katikati ni Mwenyekiti wa TASWA Arusha, Jamila Omar akioongea na waandishi wa habari
Na  Woinde Shizza,Arusha
Tamasha la waandishi wa habari, kanda ya kaskazini, linatarajiwa kufanyika jumapili, octobar 15 katika uwanja wa General Tyre ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Katika tamasha hilo, ambalo litashirikisha wanahabari zaidi ya 500, kutoka mikoa ya Arusha, Tanga, Manyara na Kilimanjaro,limedhaminiwa na shirika la hifadhi za Taifa(TANAPA) Mifuko ya hifadhi ya Jamii ya LAPF na PSPF, Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, kampuni ya vinywaji baridi ya Coca cola na kampuni ya ya vinywaji baridi ya SBC (T) Limited na Palace Hoteli.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Katibu wa TASWA mkoa wa Arusha, Mussa Juma, alisema tamasha hilo, limeandaliwa na TASWA kwa kushirikiana na kampuni ya Arusha media na maandalizi yote yamekamilika.

Juma alisema katika tamasha hilo, bingwa atazawadiwa kikombe na fedha taslimu jumla ya shilingi 500,000, mshindi wa pili fedha taslimu 100,000 na kwa upande wea mpira wa pete mshindi ni kikombe na fedha taslimu jumlaya sh 300,000 na mshindi wa pili sh 50,000.

Alisema pia kutakuwa na michezo ya mbio za magunia, kuvuta kamba, mbio za vijiko, riadha na masumbwi ambapo tayari waambuzi wanaotambuliwa na mashirika mbali mbali ya michezo watakuwepo.

Hata hivyo, alisema wadhamini wengine wa tamasha hilo wanatarajiwa kutangazwa, ili kuhakikisha wanahabari wanaburudika ambapo pia kuwa kuwa na benki maalum ambayo itatumnbuiza siku za tamasha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TASWA Arusha, Jamila Omar alitoa wito kwa wanahabari wote na familia zao kujitokeza katika tamasha hili ambalo hufanyika kila mwaka mkoani Arusha.

Alisema kauli mbio ya tamasha hilo, ambalo linaendama na maadhimisho ya kumbukumbu ya mwalimu nyerere ni michezo ni ajira, michezo ni kazi tufanye kazi kwa bidii kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya viwanda.

Mratibu wa Tamasha hilo, Andrea Ngobole alizitaja timu ambazo zitashiriki kuwa ni TASWA Dar es Salaam, Triple A,RadioSunrise , chuo cha uandishi habari cha Arusha(AJTC)timu ya Arusha One Fm, TASWA Arusha,Radio ORS ya Manyara ,NSSF na timu ya Wazee Klabu.

SINGIDA YAMUENZI MWALIMU NYERERE KWA KUSIMAMIA UBORA WA ELIMU.

 
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akiwafundisha uzalendo kwa taifa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwakichenche iliyoko wilayani Singida kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akikata utepe kama ishara ya kuzindua bweni la Sekondari ya Mtinko iliyoko wilayani Singida kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, Bweni hilo lililojengwa kwa fedha kutoka serikali kuu kupitia mradi wa Lipa kutokana na matokeo  limepewa jina la Dkt Rehema Nchimbi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akikakua ujenzi wa vyoo katika Shule ya Msingi Mwakichenche iliyoko wilayani Singida kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere. Vyoo hivyo vimejengwa kwa fedha kutoka serikali kuu kupitia program ya Lipa kutokana na Matokeo.
Kiongozi wa Wanafunzi wa Sekondari ya Ilongero Daudi William Kihanga akiishukuru serikali kuu kupitia program ya Lipa kutokana na Matokeo kwa kuwaboreshea miundombinu ya kujifunzia. Aidha ameshukuru Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi kwa kuwanunulia chakula (mchele kilo 140) kama sehemu ya maadhimisho hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi leo amekagua miradi ya uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia na Kufundishia katika shule nne za Msingi na sekondari, kama sehemu ya kumbukumbu ya Hayati baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Katika ziara yake Dkt Nchimbi ametumia muda mwingi kuwafundisha uzalendo kwa taifa, wanafunzi wa shule za Sekondari Ilongero na Mtinko pamoja na shule za Msingi Mtinko na Mwakichenche zote za Halmashauri ya Wilaya ya Singida.

Dkt Nchimbi amesema, wanafunzi hao watamuenzi mwalimu Nyerere na kudumisha uzalendo endapo watasoma kwa bidii ili taifa lipate wataalamu wa kutosha katika Nyanja mbalimbali watakaoweza kusaidia kukuza uchumi wa Tanzania.

“Mchango wa baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa taifa letu ni mkubwa sana kwakuwa licha ya kutupatia uhuru pia ametukomboa katika umasikini, ujinga na maradhi, hivyo basi nawaasa muipende sana elimu ili na nyinyi muweze kuwa sehemu ya kulisaidia taifa”, ameeleza Dkt Nchimbi.

Ameongeza kuwa katika kuboresha elimu serikali ya awamu ya tano imetoa zaidi ya shilingi bilioni 1 Mkoani Singida kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kidato cha tano na sita pamoja na kujenga miundombinu ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa kipindi cha mwaka 2017/2018.

“Tunapomkumbuka Mwalimu Nyerere leo tuthamini mchango wa serikali yetu unaofanya kwa ajili ya kuboresha sekta mbalimbali, mfano katika sekta ya elimu shilingi 1,052, 200,000 zilizotolewa nimethibitisha zimefanya kazi nzuri, kazi kwenu walimu kufundisha kwa bidii na wanafunzi kukazana katika kusoma kwakuwa mazingira yameboreshwa sana”, amesisitiza Dkt Nchimbi.

Aidha Dkt Nchimbi amewapongeza wakuu wa shule na kamati za shule hizo kwa kuchagua mafundi wazawa ambao wametumia gharama nafuu na kujenga miradi hiyo kwa kiwango kizuri, huku akisisitiza wananchi wasijicheleweshee maendeleo kwa kungoja wataalamu kutoka nje ya nchi wakati mtanzania anaweza kufanya jambo hilo kwa ubora ule ule.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Rashidi Mandoa amesema serikali kuu kupitia program ya lipa kutokana na matokeo imetoa fedha hizo kwa ajili ya shule tatu za Sekondari na mbili za Msingi ili kuinua ubora wa elimu Wilayani hapo.

Mandoa amesema kupitia miradi hiyo inayotekelezwa katika sekondari za Mtinko, Ilongero na Mwanamwema Shein pamoja na shule za Msingi za Mtinko na Mwakichenche, wananchi wameongeza imani na matumaini makubwa kwa serikali yao.

Kwa Upande wake Kiongozi wa Wanafunzi wa Sekondari ya Ilongero Daudi William Kihanga amesema nafasi waliyonayo katika kumuenzi baba wa Taifa ni kusoma kwa bidii kwakuwa wana imani kuwa kila mwalimu anapenda mwanafunzi asome kwa bidii vivyo hivyo wakisoma kwa bidii watakuwa wanamuenzi baba wa Taifa.

Kihanga ameishukuru serikali kwa kuboresha miundombinu ya kujifunzia kwakuwa inawapa wanafunzi hamasa ya kusoma kwa bidii bila kikwazo chochote.

OPERESHENI YA KUWAPIMA MACHO WAKAZI WOTE WA SINGIDA KUANZISHWA.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akipokea kifaa cha kisasa cha vipimo vya macho aina ya Auto Perimeter Glautefield Lite kutoka kwa Shirika la Sight Saver, aliyeshika kipaza sauti ni Meneja Mipango na Uendeshaji wa Shirika la Sight Savers Nchini Mhandisi Koronel Kema.

Daktari wa macho akimfanyia uchunguzi wa macho mmoja kati ya wagonjwa waliojitokeza katika maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho Mkoani Singida.

Mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho Said Mwiru akimuonyesha Mkuu wa Mkoa wa Singida (hayupo pichani) kuwa anaweza kuona na kuwatambua watu kwa kutumia jicho alilofanyiwa upasuaji. Kabla ya upasuaji huo Mwiru amesema jicho hilo lililkuwa halioni.

Baadhi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa macho wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida (hayupo pichani) katika maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho Duniani, akina mama hao wamefanyiwa upasuaji kwa hisani ya shirika la Sight savers.
MKUU wa Mkoa wa Singida, Dkt Rehema Nchimbi amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa kuanzisha operesheni maalumu ya kuwapima macho wakazi wote Mkoani hapa hususani watumishi wa serikali.

Dkt Nchimbi ametoa agizo hilo mapema jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho Duniani ambapo asilimia 94 ya watu wenye upofu Mkoani Singida wanasumbuliwa na matatizo ya macho ambayo yanazuilika.

Amesema ili watumishi wa umma waweze kutoa huduma iliyo bora wanatakiwa kuwa na uoni mzuri hivyo kuwapima ni hatua kubwa itakayosaidia kutibu na kuzuia upofu mapema.

“Mganga Mkuu wa Mkoa sasa tunataka uanzishe operesheni tupimwe wote macho, inasikitisha kusikia hao wote waliopata upofu takribani watu elfu 25 wangeweza kupona endapo wangegundulika mapema kwakuwa matatizo yaliyowasababishia upofu yanazuilika”, amesema Dkt Nchimbi na kusisitiza kuwa,

“Halmashauri zote tengeni bajeti za kununua dawa za macho pamoja na kuhakikisha wananchi wenu wote wanapimwa macho ili magonjwa yanayozuilika yapewe matibabu mapema, watendaji msione fahari kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa macho wakati mngeweza kuwasiadia”, ameeleza Dkt Nchimbi.

Awali, Dkt Nchimbi amepokea kifaa cha kisasa aina ya Auto Perimeter Glautefield Lite kutoka kwa Shirika la Sight Saver, chenye uwezo wa kuona taswira na matatizo ya macho vizuri, ambacho kwa nchi nzima kinapatikana mkoani Singida peke yake.

Amesema kifaa hicho kitawasaidi madaktari bingwa wa macho Mkoani hapa kutoa huduma bora huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili wapatiwe huduma kwani uwepo wa kifaa hicho bila kutumika kitakuwa hakina manufaa.

Dkt Nchimbi ameongeza kuwa, kutokunywa maji ya kutosha husababisha uoni hafifu ambao hupelekea upofu unaozuilika, hivyo amelishauri shirika la Sight Savers kuweka mpango wa kuboresha upatikanaji wa maji na kufanya utafiti hasa maofisini endapo watumishi wanakunywa maji ya kutosha kwakuwa yanasaidia kuzuia upofu.

Kwa upande wake Meneja Mipango na Uendeshaji wa Shirika la Sight Savers Nchini Mhandisi Koronel Kema amesema shirika hilo limeanzisha mradi wa kuboresha huduma za macho mkoani Singida utakaogharimu shilingi bilioni 2.8, mradi utakaodumu kwa muda wa miaka minne.

Kema amesema mradi huo utafadhili ujenzi wa kliniki za macho katika halmashauri za Iramba, Manyoni na Halmashauri ya Wilaya ya Singida na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ili waweze kutumia vifaa vyenye thamani ya milioni 300 ambavyo vimetolewa na shirika hilo.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Singida umeongezewa mradi mwingine utakao anza mapema mwakani na kuhusisha upimaji wa wananfunzi wote na walimu wao mashuleni ili kuweza kutibu na kuzuia upofu katika hatua za awali.

Mmoja wa wagonjwa Said Mwiru aliyefanyiwa upasuaji katika jicho lake kwenye maadhimisho hayo amemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa kabla ya upasuaji huo hakuweza kuona chochote ila siku moja baada ya matibabu hayo anaweza kuona vizuri.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Salum Manyatta amesema ataongeza kasi katika kutekeleza agizo la mkuu wa Mkoa kwakuwa walikua tayari wameshaanza kuwapima watumishi katika baadhi ya halmashauri.

Manyatta amesema zoezi lililofanyika la upimaji watumishi katika halmashauri ya Wilaya ya Manyoni limebainisha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watumishi hao walikuwa na matatizo ya macho ambayo yangepelekea upofu.

Katika kuadhimisha siku ya afya ya macho duniani, shirika la Sight Savers limeendesha zoezi la upimaji wa macho kwa watu 200 Mkoani hapa ambapo 84 kati yao wamegundulika kuwa na tatizo la macho linalosababisha wapoteze uwezo wa kuona, huku Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ikiwa ni ‘Afya ya Macho kwa wote’.

UKATAJI MITI NA UCHOMAJI MISTU NI TATIZO MKOANI GEITA.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga akisalimiana na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ambaye ni mkurugenzi msaidizi wa Idara ya usalama wa chakula kwenye wizara hiyo Bi Josephine Amulo wakati alipowasili kwenye viwanja vya ccm kalangalala.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga,akipatiwa maelezo na mtaalum kutoka kwa wakala wa usambazaji wa mbegu wakati alipotembelea Banda hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga akiwa kwenye moja kati ya mabanda ambayo yanahusika na uuzaji wa mbegu bora za kilimo.
Afisa uhusiano wa Tanesco Mkoa wa Geita Emma Nyaki akimuelezea kamanda wa jeshi la zima moto Mkoani Geita wakati alipotembelea banda ilo kwaajili ya kuona shughuli na utendaji kazi wa shirika la Tanesco Mkoani Humo.
Baadhi ya viongozi wa Wilaya wakitazama namna ambavyo jiko la kupikia la umeme linavyoweza kutumia umeme mdogo zaidi.
Afisa wa Tanesco Makao makuu Bi,Jennifer Mgendi akimuelezea Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga namna ambavyo wameendelea kutoa huduma kwa wananchi wakati  alipo tembelea  banda h la shirika hilo.
Mgeni Rasmi akipewa maelekezo ya namna ya kutumia kifaa endapo kama mteja akawa na nyumba ndogo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga akiwa kwenye banda la TFDA.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga akiwa kwenye banda la dawa zinazotokana na miti.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ambaye ni mkurugenzi msaidizi wa Idara ya usalama wa chakula kwenye wizara hiyo Bi Josephine Amulo akielezea umuhimu wa siku hiyo.
Wananchi wakiwa kwenye viwanja vya kalangalala wakifuatilia maadhimisho.
Brother K wa kikundi cha sanaa cha Futuhi akionesha makeke yake.

PICHA NA JOEL MADUKA

Serikali Mkoani Geita imeziagiza Halmashauri zote Mkoani humo kuendelea kupambana na ukataji miti na uchomaji ovyo mistu ili kupunguza athari za kimazingira zinazoathiri uzalishaji na upatikanaji wa chakula.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya Chakula itakayoadhimishwa Kitaifa mkoani Geita, Mkuu wa mkoa huo Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga amesema ni vema wakulima wakazingatia kilimo bora kwa kulima maeneo madogo ili kuboresha mazingira.

 Mkuu huyo wa Mkoa ameendelea kuwasisitiza wananchi kutumia fursa ya maonesho kwa ajili ya kujifunza mbinu mbalimbali za kuendeleza sekta ya kilimo.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ambaye ni mkurugenzi msaidizi wa Idara ya usalama wa chakula kwenye wizara hiyo Bi Josephine Amulo ameelezea madhumuni ya siku ya chakula duniani ni kuongeza ufanisi kwenye sekta ya kilimo.

Kaulimbiu ya siku ya chakula duniani kwa mwaka huu ni, Badili Mwelekeo wa Uhamaji Wekeza katika usalama wa chakula na Maendeleo Vijijini ambapo kilele cha maadhimisho hayo ni Oktoba 16 mwaka huu na mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Kilimo Dr Charles Tizeba.


Friday, October 13, 2017

HILI HAPA SULUHISHO KWA MADAKTARI WANAO UMIA KAZINI.

Mganga Mkuu mkoani Mwanza Dkt.Leonard Subby.
Madaktari pamoja na Waganga nchini wametakiwa kutumia weledi wa taaluma yao katika kuhudumia wagonjwa hususani wafanyakazi wanaoumia kazini kwa kuhakikisha wanapata huduma kwa wakati.



Mganga Mkuu mkoani Mwanza Dkt.Leonard Subby ameyasema hayo leo wakati akifunga mafunzo ya siku tano kwa madaktari na waganga kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa yaliyoandaliwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi nchini WCF na kufanyika katika ukumbi wa BOT Jijini Mwanza.



Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Madaktari pamoja na Waganga ili kutambua namna bora ya kufanya tathimini kwa mfanyakazi aliyeumia akiwa kazini.


Dkt.Abisalam Omary ambaye ni Mkurugenzi wa huduma za tiba na tathimini WCF, amesema mfuko huo unawajengea uwezo madaktari hao ili kufanya tathmini sahihi kwa wagonjwa wanaoumia kazini ama wasaidizi wao.
Rehema Kabongo ni Meneja wa Mafao ya Fidia Mfuko wa Fidia Kwa wafanyakazi (WCF) anasema kuwa "Tangu mpango huo ulipoanza mwaka 2015 kila uchwao maajiri wamekuwa wakifumbuka macho na kuona haja ya kujiunga na mfuko wa fidia kwa wafanyakazi kiasi kwamba wengi kwa makundi wameanza kujiunga na mfuko"

"Bado tunapata changamoto katika kutoa elimu kwa sababu mfuko huu bado ni mpya lakini tumejipanga kuhakikisha tunawafikia mmoja mmoja au kwa makundi ili kufikia malengo tuliyojiwekea yenye tija kwa matabibu wetu"
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba WCF, Dr. Abdullssalaam Omary akitoa maelezo kwa ufupi jinsi mfuko huo ulivyonuia kuleta mabadiliko kwa watumishi sekta ya afya.
“Tunataka hawa  madaktari wawe na ujuzi wa kutosha utakaowawezesha kufanikisha azma yetu, na tumeamua kuwa mafunzo ya aina hii yatakuwa endelevu ikiwa ni pamoja na kuwapatia muongozo utakaowasaidia kutekeleza majukumu yao ya kufanya tathmini,” alisema.
Mbali na madaktari na watumishi walio katika sekta ya afya wengi wa wafanyakazi waliopatwa na matatizo hayo kazini wanatoka sekta mbali mbali kama migodi, viwanda na usafirishaji. 

Mfuko huo umeingia mkataba na watoa huduma za afya kwenye hospitali na  vituo vya afya  zaidi ya 6,000 nchi nzima ambapo zitahudumia wafanyakazi hao.
Mgeni rasmi, Mganga Mkuu wa mkoa wa Mwanza Dkt.Leonard Subi akifunga mafunzo hayo hii leo.
Sehemu ya wadau washiriki wa mafunzo.
Mganga Mkuu mkoani Mwanza Dkt.Leonard Subby akimkabidhi cheti cha ushiriki wa mafunzo ya huduma za tiba Dr. Christopher Juma kutoka Hospitali ya Nyamagana baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo.
Mganga Mkuu mkoani Mwanza Dkt.Leonard Subby akimkabidhi cheti cha ushiriki wa mafunzo ya huduma za tiba Dr. Christina Nyandwi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo.
Mganga Mkuu mkoani Mwanza Dkt.Leonard Subby akimkabidhi cheti cha ushiriki wa mafunzo ya huduma za tiba Dr. Frighton Rwechungura kutoka Hospitali ya Nyakahanga baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo.
Mganga Mkuu mkoani Mwanza Dkt.Leonard Subby akimkabidhi cheti cha ushiriki wa mafunzo ya huduma za tiba Dr. Boniphace P. Mayala kutoka Hospitali ya Rulenge baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo.
Hongera mdau wa afya baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo.
Hongera mdau wa afya baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo.