KARIBU KISIWA CHA RUBONDO

KARIBU KISIWA CHA RUBONDO

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, August 24, 2016

MWADUI YATOKA VICHWA CHINI CCM KIRUMBA, YABAMIZWA 1-0 NA TOTO AFRICANS.

Kikosi cha Toto African.
TIMU ya Toto African ya Mwanza imeanza vyema Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga.

Mfungaji wa bao la pekee kwa Toto African alikuwa, Waziri Junior dakika ya 36 aliyemshinda mbio beki wa Mwadui na kufumua shuti maridhawa lililomshinda kipa wa Mwadui Shahban Kadri na kutinga nyavuni. 


Huo unakuwa mwanzo mzuri kwa kocha Rogasian Kaijage aliyechukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa kocha wa timu hiyo John Tegete aliyeondolewa baada ya msimu uliopita kumalizika – na mwanzo mbaya wa kocha wa Mwadui, mwenye tambo na maneno mengi Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.

Kikosi cha Mwadui Fc.

Mabadiliko ya Toto African ndani ya ungwe ya kipindi cha pili, Frank Sekule (9) anaingia badala ya Hamad Mbumba anayetoka (25), pembeni kushoto anaonekana kocha wa Mwadui Fc Jamhuri Kihwelo.


Hadi mwisho wa mchezo mashabiki walishuhudia Mwadui Fc wakitoka vichwa chini mara baada ya kukomelewa bao 1-0 dhidi ya Toto African ya Mwanza.

BARASS BINGWA Airtel Rising STARS MWANZA.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dr. Leonard Masale (katikati) akimkabidhi kombe la ubingwa nahodha wa Barass Sports Centre baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa Airtel Rising Stars mkoa wa Mwanza juzi. Kushoto ni Meneja wa Airtel Kanda ya Ziwa Ezekiel Nengwa.
Wachezaji wa Barass Sports Centre kabla ya mchezo wa fainali dhidi ya Hamas ambapo walishinda 6-1 na kutwaa uchampioni wa Airtel Rising Stars mkoani Mwanza.

Barass Bingwa Airtel Rising Stars Mwanza
Timu ya wavulana ya Barass Sports Center imetawazwa kuwa bingwa wa mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars mkoa wa Mwanza baada ya kuiadhibu Hamas Sports Center 6-1 katika mechi ya fainali iliyofanyika kwenye uwanja wa DIT nje kidogo ya jiji la Mwanza.

Mechi hiyo ilitanguliwa na mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu uliozikutanisha timu za Nyamagana United na HHT ambapo Nyamagana waliibuka na ushindi mwembamba wa 1-0. Goli hilo pekee lilifungwa na Khalifan Kamanga katika dakika ya 50.

Katika mchezo wa fainali, Hamas Sports Center ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata goli katika dakika ya 10 lililowekwa kimiani na Rogose Albert kwa shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Barass Sports Center.

Kuona hivyo Barass walikuja juu na kulisakama lango la wapinzani wao kama nyuki na kufanikiwa kupata goli la kusawazisha katika dakika ya 13 kupitia kwa Celuha Nehemia aliyefanya kazi ya ziada kupangua ngome ya Hamas kabla ya kuweka mpira wavuni.

Hamas walifanya mashambuli ya nguvu kwa nia ya kupata goli linguine lakini juhudi zao hakuzaa matunda na kujikuta wakifungwa goli la pili. Goli hili lilifunfuwa na mshambuliaji machachari Frank Osoro katika dakika ya 27.

Alikuwa ni Osoro tena aliyewainua mashabiki wa Barass Center baada ya kuwatoka walinzi wa Hamas na kufunga goli la tatu zikiwa zimebakia dakika mbili tu kabla ya kumaliza kipindi cha kwanza.

Barass walikianza kipindi cha pili kwa kasi na kufanikiwa kupata goli la nne katika dakika ya 55 kupitia kwa Maseke Mabigi ambaye alishirikiana vizuri na washambuliaji wenzake na kuachia shuti iliyojaa wavuni hivyo kuwakatisha tamaa wapinzani wao.

Mabigi ambaye alikuwa mwiba mkali kwa walinzi wa Hamas alifanikiwa kufunga goli la tano katika dakika ya 63 kabla ya Deo Martine kuhitimisha karamu hiyo ya magoli kwa kufunga goli la sita mnamo dakika ya 77.

Mechi za mashindano hiyo zimewawezesha makocha kuchangua kombaini ya wavulana ambayo itawakilisha mkoa wa Mwanza katika fainali za Airtel Rising Stars ngazi ya taifa zinazotarajiwa kufanyika kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam kuanzia September 6 hadi 11.


Timu zitakazoshiriki fainali hizo zitatoka Ilala, Kinondoni, Temeke, Zanzibar, Morogoro, Mbeya, Lindi, Mwanza na Arusha. 

KAMA UNA NDOTO ZA KUWA DIAMOND PLATNUMZ HII HAPA SIRI IMEFICHULIWA.

ERIC OMONDI HOW TO BE DIAMOND PLATNUMZ

ESRF NA UNDP/UNEP WAANDAA KONGAMANO LA KILIMO BIASHARA KANDA YA ZIWA, BURE JUMAMOSI HII


Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) ikishirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP/UNEP inaandaa Kongamano la siku moja kuhusu KILIMO BIASHARA katika KANDA YA ZIWA litakalofanyika Jijini Mwanza siku ya Jumamosi tarehe 27/8/2016 katika Ukumbi wa ROCK CITY MALL ghorofa ya tatu kuanzia saa mbili na nusu (2:30) asubuhi. Malelezo Zaidi bofya hapahttp://esrf.or.tz/ebrief/067.html Au soma kipeperushi hapa chini.

Airtel Money YAGAWA BILIONI 3 KWA WATEJA NA MAWAKALA.

Kulia Meneja wa Airtel Money Bw, Asupya Nalingigwa akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi Mr Money wa Airtel Money atakavyogawa faida ya shilingi billion 3 kwa wateja wa Airtel Money na mawakala wake nchi nzima ikiwa ni faida yao kutokana na kutumia Airtel Money kuanzia Januari hadi juni mwaka huu kushoto ni Meneja wa uhusiano wa Airtel Bw, Jackson Mmbando jana.
Kushoto ni Meneja Uhusiano wa Airtel Jackson Mmbando akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mpango wa kugawa gawio la faida ya shilingi billion 3 kwa wateja wa Airtel Money na mawakala wake nchi nzima ikiwa ni faida yao kutokana na kutumia Airtel Money kuanzia Januari hadi juni mwaka huu. Kulia ni Meneja wa Airtel Money Bw, Asupya Nalingigwa jana.
Press Release

Airtel Money yagawa billion 3 kwa wateja na Mawakala

Dar es Salaam, Jumanne 23 Agosti 2016, Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel leo imetoa gawio la faida la kila kiasi cha shilingi billion 3 kwa wateja wake wa Airtel Money na mawakala wakubwa na wadogo nchi nzima

Airtel imetoa gawio la faida kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi juni mwaka huu ambapo kila mteja atalipwa sehemu ya faida kulingana na kiasi cha salio lake katika akaunti yake ya Airtel Money kila siku

Akiongea na waandishi wa habari , Meneja Uhusiano wa Airtel Bw, Jackson Mmbando alisema “Tunayofuraha kutoa gawio la faida la shilingi bilioni 3 kwa wateja wetu na wakala nchi nzima. Tunaamini gawio hili la faida litawawezesha wateja wetu kutatua mahitaji yao ya kifedha na hivyo kuthibitisha dhamira yetu ya kuendelea kutoa huduma za kifedha”

“Tumejipanga kuwawezesha wateja wetu kwa kupitia huduma na bidhaa tunazozitoa. huduma ya Airtel Money imelenga kuleta unafuu na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha katika maeneo mbalimbali nchini hususani ya maeneo ya pembezo mwa nchi. Aliongeza Mmbando

Mpaka sasa Airtel imeshatoa kiasi cha shilingi billion 10 kwa wateja na mawakala wa Airtel money tangu  2014

MBUNGE MAHMOUD MGIMWA AKABIDHI MIFUKO 100 YA SARUJI NA NDOO KUMI ZA RAJI ZENYE UJAZO WA LITA ISHIRINI KWA SHULE YA SEKONDARI YA MDABULO.MBUNGE wa jimbo la mufindi kaskazini Mahamood Mgimwa akihutubia wananchi waliofika kwenye mkutano uliyafanyika kwenye shule ya sekondary Mdabulo.
Baadhi ya wananchi waliokuwa wamehudhuria mkutano huu wa mbunge wa jimbo la mufindi kaskazini mahamood mgimwa.
MBUNGE wa jimbo la mufindi kaskazini Mahamood Mgimwa akikabidhi mifuko 100 ya saruji na ndoo kumi za rangi zenye ujazo wa lita ishirini kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya ya kukarabati majengo ya shule ya sekondari ya Mdabulo kwa uongozi wa wilaya ya mufindi.

Na fredy mgunda,mufindi

MBUNGE wa jimbo la mufindi kaskazini Mahamood Mgimwa amekabidhi mifuko 100 ya saruji na ndoo kumi za rangi zenye ujazo wa lita ishirini kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya ya kukarabati majengo ya shule ya sekondari ya Mdabulo iliyopo Kijiji cha Mdabulo wilayani mufindi.Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Mdabulo, alisema kuweza kujenga jamii imara ni lazima kuhakikisha elimu inapewa kipaumbele cha pekee.“Sina budi kuunga mkono juhudi zenu za ujenzi wa Shule ya sekondari ya Mdabulo, ambayo imejengwa kwa nguvu za wananchi, nami kama mwakilishi wetu ninaungana nanyi kwa dhati na katika hili napenda kukabidhi mifuko ya saruji.

huo.


Alisema lengo la kutoa msaada huo, ni kutokana na shule hiyo kuwa chakavu katika maeneo muhimu kama kwenye mabweni na bwalo ambalo hutumiwa na wanafunzi kwa ajili ya chakula.


“Baada ya kupata taarifa hizi, nimeamua kuja na mkuu wa wilaya pamoja na mkurugenzi ili waangalie namna ya kufanya marekebisho katika madarasa pamoja na mabweni ya shule hii na nimewaagiza wahakikishe wanakarabati shule hiyo na iwe kwenye viwango vinavyotakiwa,” alisema Mgimwa.


Mgimwa aliwataka wanafunzi wasome kwa bidii ili waweze kufaulu na si kusoma ili kupata ajira kama ilivyozoeleka kwa watu wengi kwani serikali inafahamu changamoto ya ajira iliyopo.


Hata hivyo aliwataka wazazi na walezi kuwalea watoto katika maadili mema huku wakisaidiana na walimu kwa kushirikiana katika nyanja ya elimu ili kupanua wingo wa ufaulu kwa wanafunzi.


“Kwa kipindi cha siku kadhaa nimekuwa na ziara katika katika jimbo langu kwa lengo la kutimiza ahadi zangu pamoja na kusikiliza kero ya wananchi na kero moja wapo ni wazazi kutowajali  wanafunzi wala kutojua maendeleo ya watoto wao pindi watokapo shule”alisema Mgimwa.


Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Geogrge Mgomba, aliwataka wanafunzi wake kusome kwa ajili ya ajira binafsi na si kutegemea ajira kutoka serikalini kwa kuwa serikali ina mzigo mkubwa.


“Wanafunzi mnatakiwa msome kwa bidii na msitegemee ajira kutoka serikalini, mtafute ajira binafsi au kujiajiri wenyewe,”alisemaKwa upande wake,mkuu wa wilaya ya mufindi Jamhuri Wiliamu, alimshukuru mbunge huyo kwa kuunga mkono juhudi za wananchi za kuinua sekta ya elimu katika wilaya hiyo.

ATEKETEA KWA MOTO AKIWA AMELALA.

Bukombe. 
Mkazi wa Kitongoji cha Bomani, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Suzana Dizama (58) amefariki dunia baada ya kuungua  na moto wa kibatari ulioshika chandarua wakati akiwa amelala.

Akizungumzia tukio hilo, kaka wa Suzana, Dabirian Kinyolo alisema jana kuwa mdogo wake alirudi nyumbani usiku akitokea kilabuni kunywa pombe, alifika na kuwasha kibatari karibu na kitanda chake jambo lililosababisha moto kushika chandarua.

Kinyolo alisema katika tukio hilo wajukuu wawili wa Suzana ambao ni Ratifa Siyajali (4) na Rehema Siyajali (2), walinusurika baada ya kukimbia kutoka ndani walipoona moto unazidi.

“Kwa sababu Suzana alikuwa amelewa sana, alishindwa kukimbia hivyo kuteketea akiwa ndani ya nyumba,” alisema Kinyolo.

Tuesday, August 23, 2016

MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NCHINI AMEPANGA KUFANYA MKUTANO WA SULUHU WA VYAMA VYA SIASA NA SERIKALI.

Msajili wa vyama vya siasa nchini jaji Fransis Mutungi amepanga kufanya mkutano wa baraza la vyama vya siasa na chama cha demokrasia na maendeleo  CHADEMA ili kutafuta suluhu ya vuguvugu la siasa linaloendelea nchini.

MPIRA WA MIGUU SASA WATENGENEZWA KUTOKA MWANZA.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akizungumza mbele ya wahitimu wa kozi ya utengenezaji mipira ya soka katika Chuo cha D.I.T Tawi la Mwanza, mara baada ya kuleta mapinduzi makubwa katika kutekeleza adhma ya Serikali ya kuwa na viwanda vya ndani vyenye tija.
Rais wa TFF Jamal Malinzi amesema "Soka dunia nzima linaendeshwa kwa muhimili mmoja unaotambulika, wenye sheria zake 17, na suala la kuzingatia katika utengenezaji mpira ni uzito wa mpira kulingana na size ya mpira, kwani kuna size 4 kwa watoto na size 5, na yote hulindwa kwa vipimo vya mzunguko na uzito vinavyotambulika. Mkitengeneza mipira yenye kukubalika kwa viwango vya FIFA na kuwa na usanifu wa kimataifa kwenye sura ya nje ya mpira mna kila sababu ya kutinga kwenye soko la kimataifa"
"Katika vitu vinavyokwamisha soka la nchi hii mbali na kuwa na changamoto ya ukosefu wa viwanja na mtaji kwa wakufunzi changamoto nyingine ni mipira. Hivyo hii ni Fursa kubwa ambayo mkiitumia mkawa na Chapa ya kwenu kwa viwango vinavyotambulika na FIFA mmeula, kwani mbali na timu za Ligi kuu pia tuna timu za Shule za msingi ambazo ni 19,300 ukipeleka mipira 10 kwa mwaka hiyo ni karibu mipira laki 2, Shule za Sekondari 5,000 ukipeleka mipira 10 kwa kila shule kwa mwaka ni mipira elfu 50, Vilabu vya nchi hii vilivyo sajiliwa na ambavyo havijasajiliwa, amachan, professional havipungui 5,000, na timu kubwa zinapokwenda kwenye mechi za kimataifa zinaenda na mipira isiyopungua 40 au pengine 50 hivyo ni kwa maandalizi ya mchezo mmoja tu, Premium League tuna timu 16, Daraja la Kwanza 24, daraja la pili 24, Kwa hiyo kwa kifupi na mahesabu ya haraka haraka tunahitaji mipira isiyopungua laki 5 kwa mwaka. Jeh hii siyo fursa?"
Alisema Rais wa TFF Jamal Malinzi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akiongoza zoezi la kukabidhi vyeti kwa wahitimu kozi ya utengenezaji mipira ya soka katika Chuo cha D.I.T Tawi la Mwanza,
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akiongoza zoezi la kukabidhi vyeti kwa wahitimu kozi ya utengenezaji mipira ya soka katika Chuo cha D.I.T Tawi la Mwanza,
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akiongoza zoezi la kukabidhi vyeti kwa wahitimu kozi ya utengenezaji mipira ya soka katika Chuo cha D.I.T Tawi la Mwanza,
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akipokea zawadi yake toka kwa mmoja wa wahitimu.
Rais wa TFF Jamal Malinzi akipokea zawadi yake toka kwa mmoja wa wahitimu.
WANAFUNZI 14 wamehitimu mafunzo ya kutengeneza mpira wa miguu yaliyotolewa kwa wiki mbili kwenye Chuo cha Taasisi ya Ufundi (D.I.T) tawi la Mwanza.
Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza wahitimu hao, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema anawapongeza wahitimu hao na wakitumia taaluma yao vizuri wataleta mabadiliko makubwa katika soka nchini.
Mongella ameahidi kushawishi wakurungenzi wa halmashauri za mkoani hapa kununua mipira hiyo iliyotengenezwa na wanafunzi hao kutoka chuo hicho ili kusaidia katika kukuza mchezo wa soka.
Mongella amewaomba wanafunzi hao waendelee kutengeneza mipira bora ili kuhakikisha mipira hiyo inatumika katika Ligi Kuu Bara.
Mongella amenunua mipira 40 kwa ajili ya kuzipa timu ya Mbao fc na Toto Africans zinazoshiriki Ligi Kuu, kila timu ikijinyakulia mipira 20. Kaimu Mkurugenzi wa TAN-TRADE, Edwin Rutageruka amekipongeza chuo hicho kwa kukubali mwito wa TanTrade katika kutoa mafunzo hayo.
Rutageruka ameiomba serikali iunge mkono juhudi za kununua bidhaa zinazotengenezwa nchini. Rutageruka ameliomba pia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lifanye utafiti kujua mahitaji ya mipira nchini na ameahidi kushirikiana na Rais wa TFF, Jamal Malinzi katika kutafuta soko la mpira wa miguu ndani na nje ya nchi.
Mkuu wa chuo hicho, tawi la Mwanza, Albert Mmari alisema wataendelea kutoa mafunzo hayo ili kuzidi kupata wataalamu zaidi na amewapongeza wahitimu wa mafunzo hayo ambao ni Abdallah Juma, Frank Nickson, Zacharia Gervas na Moukthtar Ahmed.
Wengine waliohitimu mafunzo hayo ni Nestory Mkumbi, Seleman Seleman, Asimwe Mganyizi, Magesa Nyakwarya, Mary Massala, Loyce Manyenye na Praxeda Lazary, Kulwa Paul, Benedicto Thomas, Malando Emmanuel, Rashid Kitambi, Clement Mange na Mouktar Ally.

MBUNGE WA ILEJE JANET MBENE ATAKA WALIOKULA FEDHA ZA MRADI WA HOSPITALI WACHUNGUZWE

 Mbunge wa Ileje Mh Janet Mbene, akiwa na watendaji wa Halmashauri hiyo  akikagua sehemu ya juu ya jengo jipya la Hospitali ya Wilaya ya Ileje Ksata ya Itumba inayojengwa kwa pesa za Serikali ya Tanzania
 Mganga mkuu wa Hospitali ya  Ileje akitoa maelezo kwa  Mbunge wa Jimbo hilo Mh Janet Mbene alipokuw akaikagua ujenzi wa jengo jipya la Hospitali hiyo
 Mbunge wa Ileje Mh Janet Mbene akitoa pole katika wodi ya Wanawake amabao walibahatika kujifungua kwa Upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Ileje.
  Mbunge wa Ileje Mh Janet Mbene akitoa pole katika wodi ya Wanawake amabao walibahatika kujifungua kwa Upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Ileje.
  Mbunge wa Ileje Mh Janet Mbene akiwa amembeba mmoja ya watoto waliozaliw akatika hospitali ya Wilaya ya Ileje

  Mbunge wa Ileje Mh Janet Mbene akikagua mashine ya X -Ray  katika Hospitali ya Wilaya ya Ileje
  Mbunge wa Ileje Mh Janet Mbene akipita katika moja za wodi za Hospitali ya Wilaya ya Ileje


    Na Mwandishiwetu,  Ileje

 MBUNGE wa Ileje  Mh Janet Mbene,  amemtaka mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo  kuwachukulia hatua wale wote ambao wamehusika katika ubadhilifu wa fedha za mradi wa ujenzi wa Hospitlai ya Wilaya ya Ileje.

Mh Mbene alisema hayo alipofanya ziara katika Hospitali hiyo na kubaini upungufu mkubwa juu ya muda wa ujenzi wa Hospitali hiyo na kiasi cha pesa kilichotolewa na Wizara ya fedha katika kaukamilisha ujenzi huo ambao kwa sasa umekwama.

"Naomba Mkurugenzi afikishe swala hili kwa TAKUKURU, hili waweze kubaini ni kiasi gani ambacho kimeibiwa na wale wote waliohusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria hasa kwa mujibu wa sheria za utumishi wa Umma na kushtakiwa katika Mamlaka zinazo husika" alisema Mbene.

aliweka wazi kuwa inaonyesha wazi kuwa wakati wa kuvunja bara za la madiwani kiasi cha pesa zaidi ya milioni 100 kilikuwepo kwenye akaunti kwa jaili ya ujenzi wa jengo jipya la Hospitali ya Wilaya ya Ileje lakini mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi na kikao cha kwanza cha baraza la Madiwani fedha hizo azionekani zilipokwenda.

anataja kuwa kumekuwa na utamaduni wa watendaji kutumia fedha kinyume na mipango hali inayfanya kukwama kwa miradi mingi katika Halmashauri hiyo.

alitoa wito kwa wananchi kuwa na imani na serikali walioichagua kwani sasa yeye kama mbunge yupo begakwabegakuakikisha anakomesha ufisadi ndani ya wilaya hiyo

MAMADOU SAKHO AREJEA MAZOEZINI, LIVERPOOL YAPANGA KUMTOA KWA MKOPO.

Beki mtata wa Liverpool, Mamadou Sakho amerejea mazoezini chini ya Kocha Jurgen Klopp baada ya kuwa nje kwa muda kutokana na kuwa majeruhi ambapo mpaka sasa ameshakosa mechi mbili za Premier League za timu yake.
Beki huyo ambaye amekuwa katika mvutano na klabu yake kutokana na matukio yake ya kuonyesha utovu wa nidhamu ikiwemo kufukuzwa katika kambi ya timu hiyo ilipokuwa Marekani, alionekana katika mazoezi ya leo akiwa na wenzake sambamba na straika wa timu hiyo, Sadio Mane ambaye alikuwa majeruhi kwa kuumia bega.

  Sakho ambaye pia alikuwa na kashfa ya kutumia dawa za kuongeza nguvu michezo inaelezwa kuwa anaweza kuwa na wakti mgumu kupata namba kikosini hapo kutokana na kuonyesha kutoivana na bosi wake huyo wa benchi la ufundi.

Wakati akiondolewa kambini Marekani, Klopp alilalamika tabia za beki huyo raia wa Ufaransa kuwa alikuwa akionyesha utovu wa nidhamu hadharani jambo ambalo lingeweza kuigawa timu wakati yeye anataka timu iwe kitu kimoja.

Wakati huohuo kuna taarifa kuwa Liverpool inafanya mpango wa kumtoa beki huyo mwenye umri wa miaka 26 kwa mkopo kwenda timu nyingine.

Klopp aliwasajili Joel Matip na Ragnar Klavan ili kuongeza nguvu katika safu ya ulinzi wa kati jambo ambalo linampa ugumu Sakho kwa kuwa pia bado Dejan Lovren ana uhakika wa kucheza katika nafasi hiyo.

HAPPY BIRTHDA BLOGGER MC BARAKA

Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, Aug 23. Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuishuhudia siku hii. Ni neema ambayo sistahili,Napaswa kutambua kwamba kila siku katika maisha yangu ni dhamana, niitumie kwa mambo mema,Nizingatie wajibu wa kuvitumia kikamilifu vipaji alivyonipa Mungu kwa manufaa ya wanadamu. 

Siwezi kujivunia chochote nilichoweza kufanya, bali ni kumshukuru Mungu na kuendelea kumtegemea na kila ninaposherehekea kumbumbuku ya siku ya kuzaliwa kwangu, fikra zinanituma kufananisha mchango wangu Kimkoa na Kitaifa sawa na ule wa watu maarufu,Ukweli ni kwamba ninajitahidi lakini mchango wangu bado ni hafifu sana. Mengi nimefanya kupitia Bukobawadau Blog Media ninachoweza kusema ni kwamba changamoto ni kubwa sana! 

I will always praise God

Monday, August 22, 2016

JESHI LA POLISI LAFUNGUKA KUHUSU ASKARI WAKE KUONEKANA KUFANYA MAZOEZI.

 Jeshi la Polisi leo limetoa ufafanuzi kuhusu Askari wake wanaoonekana kufanya mazoezi sehemu mbalimbali nchini kuwa ni kawaida kwa Jeshi hilo kufanya hivyo.

Jeshi hilo limesema ni utaratibu wa vikosi vyake kufanya mazoezi ya wazi.

Mazoezi hayo yamefanyika katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Singida, Mwanza na Mtwara.

Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi mkoani Singida Mayala Towo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi pamoja na Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara Thobias Sedoyeka wameeleza dhima ya mazoezi hayo.

ZIFUATAZO NI KAULI ZA MAKAMANDA WA MIKOA ILIYOHUSISHWA NA MAZOEZI HAYO.

MAYALA TOWO - SINGIDA

"Ni vizuri wananchi wakayaona mazoezi ya jshi lao yako vipi, tukifanya usiku itakuwa ni wakati wamelala au tunaweza kuwapa hofu zaidi na nyie waandishi wa Habari mtakuwa mmelala, hata leo mmejitokeza kwa kuwa mmetuona tuko kimazoezi"

Kisha akaongeza " Jeshi linaundwa na wananchi wenyewe na wanalipwa mishahara na Serikali, ni kodi zao zinawalipa, kwa hiyo tukaona ni vyema watuone kukiwa kumekucha ili wajue kodi zao zinakwenda wapi, na wanaotulinda wakoje....!!!"

AHMED MSANGI - MWANZA
"Siku zote unafanya mazoezi porini, saa nyingine yatupasa kufanya mijini, hivyo tunafanya mazoezi kulingana na michoro ya mjini, tupite tuone mji uko vipi na maeneo kama hayo yako vipi. Kwa hiyo hayo ni mazoezi ya kawaida tu! Siyo ya kumtisha mtu" alisema Kamanda Msangi na kisha kuongeza

" Wengine wanasema kwanini wanafanya mazoezi hadharani? Hatuwezi kujiweka vichakani muda wote lazima saa nyingine tuuvae uasilia, tutinge ndani ya mji"

THOBIAS SEDOYEKA - MTWARA.
"Wananchi wasiwe na hofu kwa milio waliyoisikia, madhumuni ya mazoezi haya ni kwaajili ya ukakamavu na pia kujipima kwa wakati wowote na kwa lolote" alisema Kamanda Sedoyeka na kisha kuongeza

" Hatuna nia mbaya na wananchi na hatuna sababu ya kukurupushana na wananchi isipokuwa waamini kuwa haya ni mazoezi ya kawaida kabisa.


Jeshi la polisi nchini limewatoa hofu wananchi kuhusiana na mazoezi yanayoendelea kufanywa na jeshi hilo katika maeneo mbalimbali ya nchi kuwa ni kawaida kwa jeshi kufanya hivyo.